Raia Wawili wa China Wakabiliwa na Kesi ya Utakatishaji Fedha T-Sh Bilioni 2.13

Raia wawili wa ambao ni wakazi wa  China Weisi Wang (41) pamoja  na Yao Licong wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi yakiwemo ya utakatishaji fedha zenye thamani ya takribani Shilingi bilioni mbili na milioni 13.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki na Mawakili wa Serikali Wakuu Patrick Mwita na Benjamin Muroto ambao waliwakilisha upande wa Jamhuri.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa na mahakamani washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la kuongoza genge la uhalifu huku wakidaiwa kutenda makosa hayo katika vipindi tofauti kati ya Desemba mosi 2024 na Desemba 30, 2025 katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza na Unguja Zanzibar pamoja na maeneo mengine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha inadaiwa kuwa washtakiwa walipanga kuandaa na kuongoza genge la kihalifu lililojihusisha na vitendo vya kughushi nyaraka, kunakili kadi za ATM, kukwepa kodi pamoja na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika shtaka la pili wanadaiwa kutenda kosa la utakatishaji fedha ambapo walimiliki Dola za Kimarekani 707,075 na Shilingi za Kitanzania 281,710,000 wakijua kuwa fedha hizo ni zao la uhalifu.

Hivyo baada ya kusomewa mashtaka hayo Hakimu Beda Nyaki alieleza kuwa washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo na  kubainisha kuwa kutokana na uzito wa mashtaka washtakiwa hao hawana sifa ya kupata dhamana katika mahakama hiyo.

Hata hivyo upande wa Jamhuri ulieleza kuwa upelelezi wa shauri bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa tena  hivyo basi Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Januari 21, 2026 kwa ajili ya kutajwa tena.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii