Waziri wa Mambo ya Ndani wa Venezuela Diosdado Cabello amesema watu 100 wameuawa katika shambulio la Marekani mnamo siku ya Jumamosi lililomuondoa Rais Nicolás Maduro madarakani.
Ambapo Serikali ya Venezuela imethibitisha kuwa wanajeshi na maafisa kadhaa wa usalama waliuawa katika uvamizi wa kijeshi uliofanywa na Marekani, ingawa haikutoa idadi kamili ya waliopoteza maisha mara moja baadaye jeshi la nchi hiyo lilichapisha orodha ya majina ya wanajeshi 23 waliothibitishwa kuuawa katika operesheni hiyo.
Maafisa wa Venezuela walisema sehemu kubwa ya kikosi cha ulinzi cha Rais Nicolás Maduro iliuawa “kwa kikatili” wakati wa uvamizi huo kwa upande wake serikali ya Cuba ilitangaza kuwa wanajeshi na maafisa wake wa kijasusi 32 waliokuwa nchini Venezuela waliuawa katika tukio hilo, jambo lililoibua taharuki kubwa katika ukanda wa Amerika ya Kusini.
Katika uvamizi huo, Rais Nicolás Maduro na mkewe Cilia Flores walikamatwa. Flores alipata jeraha la kichwa huku Maduro akijeruhiwa mguuni kwa mujibu wa taarifa za maafisa wa Venezuela.
Kufuatia vifo hivyo Rais wa mpito wa Venezuela Delcy Rodríguez Jumanne iliyopita alitangaza wiki moja ya maombolezo ya kitaifa kuwaenzi wanajeshi waliouawa katika uvamizi huo wa kijeshi.
Tukio hilo limeendelea kuzua mjadala na mvutano wa kimataifa huku mataifa kadhaa yakitoa wito wa kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa na kulindwa kwa raia pamoja na wanajeshi wasiohusika moja kwa moja katika mapigano.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime