Somalia yalaani ziara ya Waziri wa mambo ya kigeni wa Israel Somaliland

Hatua ya Waziri wa Mambo ya nje wa Israel Gideon Saar kuzuru jimbo la Somaliland siku 10 baada ya kulitambua jimbo hilo kama nchi huru, imeshtumiwa vikali na Somalia ambayo imetaja kitendo hicho kama kisichokubalika

Waziri Saar alizuru Somaliland siku ya Jumanne na kupokelewa na viongozi waandamizi wa jimbo hilo, huku akisema hatua ya Israeli kulitambua jimbo hilo kama taifa, ulikuwa ni uamuzi sahihi wa kufanya.

Kiongozi wa Somaliland, Abdirahman Abdullahi Mohamed, baada ya kukutana na Waziri Saar ameisifu Israel kwa uamuzi wake wa kijasiri ambao amesema, unafungua ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo.

Wakati wa ziara hiyo fupi, usalama uliimarishwa mjini Hargeisa, huku watu wa kawaida, wakiwekewa vikwazo vya kutembea kwa uhuru.

Hata hivyo, serikali ya Somalia, ambayo inaendelea kusisitiza kuwa jimbo la Somaliland ambalo lilijitangazia uhuru wake na kujitenga mwaka 1991, bado  ni sehemu yake, imekasirishwa sana na ziara hiyo, ambayo imesema ni kinyume cha sheria na haikubaliki.

Umoja wa Afrika na mataifa mbalimbali, yamelaani hatua ya Israel, ikisisitiza kuwa Somaliland inasalia sehemu ya Somalia.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii