Afisa Mnadhimu wa kitengo cha usalama barabarani Makao Makuu ya Polisi Dar-es- Salaam- SACP Butusyo Akim Mwambelo amewataka waendesha vyombo vya moto kuzingatia sheria wakati wanapoendesha vyombo vyao kwa kuacha kupokea simu na badala yake kusimamisha chombo chake ili kusikiliza simu hiyo jambo ambalo litasaidia kupunguza ajali barabarani.
Akizungumza na Madereva wanaondesha vyombo vya moto wakiwemo Maafisa usafirishaji (Bodaboda), Bajaji na waendesha Bajaji za mizingo (Guta) huko katika Uwanja wa Polisi Mabatini, Wilaya ya Nyamagana, Mkoa wa Mwanza, amewaasa madereva hao kufanya biashara kwa upendo kwa kugawana abiria na sio kuzidisha abiria ili tu waweze kupata kipato "lazima kila mmoja wenu aweze kugawana kipato na wenziwe kwani hili linawezekana kukiwa na upendo"
Vilevile Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu ya kikosi cha Usalama barabarani ASP-Mwashamba Rashid Onesmo amewaasa madereva hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani wakati wanaendesha chombo cha moto ili kuepusha ajali zisizotarajiwa.
Aidha amewasisitiza kusoma kwa ajili ya kupata leseni hai katika vyuo vinavyotambulika kisheria, ili kuepuka udanganyifu pamoja na kukosa leseni inayotambulika kisheria.
Naye, mmoja wa madereva hao Abdallah Bakari amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuja kutoa elimu hiyo kwani kuna baadhi ya madereva hawajui sheria za usalama barabarani, na kuhakikisha kuwa elimu hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali za barabarani.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime