Katika oparesheni maalum inayoendelea mkoani Geita, Idara ya Uhamiaji imefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 126 kutoka nchini Burundi wengi wao wakiwa ni vijana ambao wapo nchini kinyume na sheria huku wakifanya shughuli za kujitafutia kipato.
Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Kamishna Msaidizi Mwandamizi, James Mwanjotile, amesema kuwa wahamiaji hao walikamatwa katika maeneo ya mjini Geita pamoja na pembezoni mwa mji, ambapo walikuwa wakiishi na kufanya kazi bila vibali halali.
Mwanjotile amesema, kwa sasa wanaendelea na taratibu za kuwapeleka wahamiaji hao makwao, huku akisisitiza kuwa oparesheni hiyo itaendelea kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Katika hatua nyingine, Mwanjotile amesema kuwa kwa robo ya mwisho ya mwaka wa fedha 2024/25, jumla ya wahamiaji haramu 593 waliondoshwa nchini, akisisitiza dhamira ya serikali kudhibiti uhamiaji haramu.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi James Mwanjotile ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa na kuelimisha jamii kuhusu madhara ya uhamiaji haramu, akisema kwamba ushirikiano huo ni muhimu katika kulinda usalama wa taifa.