Marekani imewafukuza wahamiaji watano kutoka nchi za Asia na Caribbean na kuwapeleka katika nchi ndogo ya kifalme ya Eswatini, barani Afrika, maafisa wametangaza Jumanne, Julai 15.
Utawala wa Trump umetangaza siku ya Jumanne kwamba umewafukuza wahamiaji haramu watano kutoka nchi za Asia na Caribbean kwenda Eswatini, nchi ndogo ya kusini mwa Afrika, kwa madai kuwa nchi yao inakataa kuwapokea.
Wahamiaji waliofukuzwa ni raia wa Cuba, Jamaica, Laos, Vietnam na Yemen. Kulingana na Idara ya Usalama wa Taifa ya Marekani, wamepatikana na hatia ya uhalifu wa kutumia nguvu kama vile ubakaji wa watoto na mauaji.
Utawala wa Trump umetetea kile kinachoitwa kufukuzwa kwa nchi ya tatu kama inavyohitajika, kwani nchi wanakotoka baadhi ya wale wanaolengwa kufukuzwa wakati mwingine hukataa kuwakubali.
Mnamo Julai 4, Marekani ilsafirisha wahamiaji haramu wanane kwenda nchini Sudan Kusini, nchi masikini na yenye migogoro, baada ya kuidhinishwa kufanya hivyo na Mahakama ya Juu baada ya mabishano ya muda mrefu ya kisheria.
"Leo, Idara ya Usalama wa Nchi imefanya uhamisho kwa ndege hadi nchi ya tatu, Eswatini," idara hiyo imesema kwenye akaunti yake ya X.
Hawa ni "wageni wahalifu haramu" ambao nchi husika zimekataa kuwapokea, imeeleza, ikichapisha utambulisho, picha, na mashtaka dhidi ya watu hao watano.
Eswatini, nchi ya kifalme ya mwisho kabisa barani Afrika, nchi jirani ya Afrika Kusini, imetawaliwa tangu 1986 na Mswati III, inayokosolewa kwa maisha yake ya kifahari na mara kwa mara inashutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu.
Rais wa Marekani Donald Trump amefanya vita dhidi ya wahamiaji haramu kuwa kipaumbele cha kwanza, akimaanisha "uvamizi" wa Marekani unaofanywa na "wahalifu kutoka nje ya nchi" na kuzungumza sana kuhusu uhamisho wa wahamiaji.
Lakini mpango wake wa kuwafukuza watu wengi umetatizwa au kupunguzwa kasi na maamuzi mengi ya mahakama, hasa kwa misingi kwamba watu wanaolengwa wanapaswa kuwa na uwezo wa kudai haki zao.