Daktari wa kuunda wanawake makalio aachiliwa kwa dhamana

DAKTARI wa masuala ya urembo aliyeshtakiwa kumuua mwanamke aliyeenda hospitali kwake kurembeshwa makalio ameachiliwa dhamana ya Sh1 milioni na mdhamini mmoja.

Dkt Robert Maweu Mutula anayeshtakiwa pamoja na wamiliki wa Hospitali ya Omnicare Medical Limited almaarufu Body By Design (BBD) George Wakaria Njoroge na muuguzi Lilian Edna Wanjiru Mwariri waliachiliwa na hakimu mwandamizi mahakama ya Kibera Samson Temu.

Endapo watashindwa kupata dhamana ya Sh1 milioni, Bw Temu aliwapa dhamana ya pesa taslimu Sh500,000 kila mmoja.

Dkt Mutula, Njoroge na Wanjiru wamekanusha shtaka la kumuua bila ya kukusudia Lucy Wambui Kamau mnamo Oktoba 16, 2024.

Akitoa uamuzi, Bw Temu alisema dhamana ni haki ya kila mshukiwa na inaweza tu kukataliwa endapo upande wa mashtaka umewasilisha ushahidi kuthibitisha wakiachiliwa kwa dhamana watatoroka.

Bw Temu aliwaachilia washtakiwa kufuatia ombi la wakili mwenye tajriba ya juu Eric Mutua aliyeeleza mahakama Dkt Mutula ni daktari wa maafisa wa kijeshi KDF na pia mwenyekiti wa St John’s Ambulance inayotoa huduma kwa Wakenya wote.

Bw Mutua alieleza mahakama kuendelea kumweka Dkt Mutula kizuizini ni kuhatarisha maisha ya wengi wanaotegemea huduma zake.

Washtakiwa hao pia wamewasilisha kesi katika mahakama kuu wakiomba DPP azimwe kuwashtaki Dkt Mutula na wenzake kwa mauaji na badala yake kesi hiyo ipelekwe kwa bodi ya KMPDC kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii