Waasi wa M23 wauteka uwanja wa ndege wa Goma, Marekani yahimiza raia wake kuondoka DRC

Kundi la waasi wa M23 Jumanne lilichukua udhibiti wa uwanja wa ndege wa mji wa Goma, chanzo cha usalama kimesema, kufuatia mapigano ya siku tatu ambayo yameua zaidi ya watu 100.

Karibu watu 1,000 walijeruhiwa pia, kulingana na takwimu zilizokusanywa na shirika la habari la AFP kutoka kwa hospitali za Goma ambazo zimezidiwa na idadi ya majeruhi.

Siku tatu za mapigano makali zimeuacha mji huo muhimu wa mashariki mwa DRC katika hali ya hatari baada ya kutekwa na waasi wa M23.

Baada ya kuingia mjini kati Goma siku ya Jumapili, mapigano ndani ya mitaa kwa kutumia mizinga na risasi yamesabisha miili ya watu kuachwa kwenye barabara za mji huo, huku wapiganaji wengi wa M23 wakiingia katika mji huo mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Ilikuwa haijafahamika wazi ni maeneo gani ya Goma ambayo yako chini ya udhibiti wa jeshi la Congo au waasi wa M23, ambao wamedai kuuteka mji huo Jumapili usiku.

Wapiganaji wa M23 walichukua udhibiti wa uwanja wa ndege Jumanne, na kuongeza kuwa “zaidi ya wanajeshi 1,200 wa Congo walijisalimisha na wamezuiliwa “kwenye kambi ya tume ya Umoja wa Mataifa nchini DRC inayopatikana kwenye uwanja wa ndege.

Hayo ya kiarifiwa, Ubalozi wa Marekani mjini Kinshasa umewataka raia wa Marekani kuondoka nchini DRC baada ya waandamanaji kushambulia balozi kadhaa kutokana na mzozo wa huko Goma.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii