Maelfu ya Wapalestina warejea Gaza City

Maelfu ya Wapalestina walimiminika kuelekea Gaza city Jumatatu, huku Israel ikifungua vituo vya ukaguzi na kuwaruhusu watu kurejea katika maeneo ya kaskazini mwa eneo hilo ambalo lilikuwa limefungwa tangu siku ya mwanzo ya vita kati ya Israel na Hamas, zaidi ya miezi 15 iliyopita.

Wapalestina, wengi wao wakitembea kwa miguu, walibeba mizigo yao walioweza kubeba walipokuwa wakirudi kuona kama nyumba zao za zamani hazikubomolewa.

Lakini sehemu kubwa ya eneo hilo iliharibika wakati wa mashambulizi ya Israel yaliyolenga wanamgambo wa Hamas na majengo yaliotekwa na kundi hilo.

Gaza city ni moja ya maeneo mengi ambako jeshi la Israel liliamuru wakazi kuondoka lilipokuwa likifanya mashambulizi yake.

Wapalestina mara nyngi walijielekeza eneo la kusini mwa Gaza, na kuambiwa baadaye kuondoka tena wakati Israel ilipofanya mashambulizi huko pia.

Wengi kati ya watu walioondoka walitoroka makazi yao mara kadhaa na kurudi kuishi ndani ya mahema katika kambi za wakimbizi.

Takriban watu milioni 1 walipewa amri ya kuondoka kaskazini mwa Gaza wakati Israel ilipoanzisha mashambulizi yake Oktoba 2023. Jeshi hadi sasa, limewazuia kurejea.

Kurejea kwa Wapalestina huko Gaza city kunajiri katika hatua za mwanzo za makubaliano ya kusitisha mapigano kwa wiki sita kati ya Israel na Hamas, ambayo yalipelekea kuachiliwa kwa mateka waliokuwa wanashikiliwa huko Gaza, kuachiliwa kwa wafungwa 300 wa Kipalestina waliokuwa wanashikiliwa na Israel na kuingizwa kwa wingi kwa misaada ya kibanadamu ndani ya Gaza.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii