Wanajeshi 20 wa Nigeria wauawa na wanamgambo wa Kiislamu

Wapiganaji wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Kiislamu waliwaua wanajeshi 20 wa Nigeria, akiwemo kamanda mmoja, baada ya kushambulia kambi ya kijeshi katika mji wa mbali kaskazini mashariki mwa jimbo la Borno, vyanzo vya usalama na wakazi walisema Jumapili.

Wapiganaji wa Boko Haram na tawi la Islamic State magharibi mwa Afrika (ISWAP) wamekuwa wakiendesha harakati zao huko Borno, wakilenga wanajeshi na raia, katika mashambulizi yao wanaua na kusababisha maelfu ya watu kutoroka makazi yao.

Shambulizi la hivi karibuni lilifanyika siku ya Ijumaa, wakati wapiganaji wa ISWAP walipowasili wakiwa kwenye malori yenye silaha na kushambulia kikosi cha 149 cha jeshi katika mji wa Malam-Fatori, njia inayoelekea kwenye mpaka na Niger, wanajeshi wawili na wakazi walisema.

Mwanajeshi mmoja aliyenusurika katika shambulizi hilo ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kwamba wanajeshi hawakutarajia shambulizi hilo huku wapiganaji hao “wakifyatua risasi nyingi kila mahali.”

“Tulijaribu kadri tuwezavyo kuzima mashambulizi na baada ya zaidi ya saa tatu za kufyatuliana risasi, walituzidi nguvu na kumua kamanda wetu mkuu mwenye cheo cha Luteni Kanali,” alisema mwanajeshi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu hana mamlaka ya kuzungumza na vyombo vya habari.

Alisema wanajeshi 20 waliuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.

Msemaji wa jeshi la Nigeria haukapatika mara moja kutoa maelezo.

Wakazi waliotoroka mji huo walisema baadhi ya wanamgambo walionekana huko Malam-Fatori Jumamosi usiku.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii