Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza kujitoa kwa Marekani kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), hatua iliyopokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa wananchi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii.
Trump amechukua uamuzi huo katika siku yake ya kwanza madarakani, akieleza kuwa Marekani inaipa WHO kiasi kikubwa cha fedha wakati China yenye watu wengi zaidi, inaipa WHO kiasi kidogo ambacho hakiendani na idadi ya raia wake.
Sababu nyingine inayotajwa kumsukuma Trump kuchukua uamuzi huo aliouanza mwaka 2020 katika muhula wake wa kwanza wa urais, ni madai kuwa WHO ilishindwa kueleza ukweli kuhusu chanzo cha Ugonjwa wa Covid 19 sambamba na kushindwa kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na ugonjwa huo.