Somalia na Ethiopia zakubaliana kumaliza mvutano kati yao

Nchi za Somalia na Ethiopia, zimekubaliana kumaliza mvutano kati yao baada ya kumalizika kwa mazungumzo yaliyoongozwa na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan jijini Ankara.

Rais Erdogan, msuluhishi wa mzozo kati ya nchi hizo mbili za pembe ya Afrika, ameelezea makubaliano hayo  kuwa ya kihistoria na kuongeza kuwa, ni hatua muhimu ya mataifa hayo jirani kushirikiana kwa amani na utulivu.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Waziri Mkuu wa EthiopiaAbiy Ahmed na rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, ambao walishiriki kwenye mazungumzo mapya, baada ya hapo awali kutozaa matunda.

Kwa karibu mwaka mmoja sasa, mataifa hayo mawili yamekuwa yakizozana baada ya hatua ya Ethipia, mwezi Januari kuingia kwenye mkataba na jimbo lililojitenga na uongozi wa Mogadishu la Somaliland, ili kutumia bandari yake na kujenga kambi ya jeshi.

Mkataba huo kati ya Ethiopia na Somaliland, uliikasirisha uongozi wa Mogadishu ambao uliamua kumrudisha nyumbani balozi wake kutoka jijini Addis Ababa, ikiishtumu nchi hiyo jirani kwa kuivamia kinyume cha sheria.

Hata hivyo, baada ya mazungumzo ya zaidia ya saa nane, siku ya Jumatano, rais Erdogan amesema kuwa viongozi wa nchi hizo mbili wamekubaliana kutatua na kumaliza tofauti zao, na kutafuta njia mwafaka ya kushirikiana, ili Ethiopia itumie Bahari ya Hindi kwa kuheshimu uhuru wa nchi ya Somalia.

Mazungumzo mengine ya namna ya kutekeleza makubaliano hayo; yanatarajiwa kuendelea mwezi Februari.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii