Rais wa kihafidhina wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol ang'ang'ania madarakani. Siku ya Alhamisi, Desemba 5, chama chake kmetangaza kwamba kitashinda hoja ya kushtakiwa iliyowasilishwa Bungeni na upinzani baada ya jaribio lake la kushindwa kulazimisha sheria ya kijeshi. Wakati huohuo, kiongozi wa chama amemtaka aondoke katika chama.
Yoon Suk-yeol alizua mshangao nchini Korea Kusini siku ya Jumanne jioni kwa kutangaza sheria ya kijeshi na kuamuru jeshi kuvamia Bunge, kabla ya kubadili kauli saa sita baadaye chini ya shinikizo kutoka kwa wabunge na waandamanaji.
Vyama sita vya upinzani viliwasilisha ombi la kumtaka rais ajiuzulu siku ya Jumatano, vikimtuhumu kwa "kukiuka Katiba na sheria." Hoja hii itapigiwa kura siku ya Jumamosi saa 3 usiku saa za Korea Kusini (sawa na saa 6 mchana saa za Afrika ya Kati ), kulingana na shirika la habari la Yonhap. Upinzani una jumla ya viti 192 kati ya 300 katika Bunge la taifa, huku wabunge wengine 108 wakiwa wa chama cha Yoon Suk-yeol cha People's Power Party (PPP).
Hoja hiyo lazima ipitishwe na kura ya thuluthi mbili ya walio wengi, hivyo basi kujitoa kwa angalau wabunge wanane kutoka chama cha rais kutakuwa muhimu ili kumuondoa malakani Yoon Suk-yeol.
Siku ya Alhamisi, kiongozi wa PPP Bungeni, Choo Kyung-ho, amethibitisha kwamba chama chake kitapiga kura ya kupinga hoja hiyo. "Wabunge wote 108 wa People's Power Party watasalia na umoja kukataa kumuondoa rais mamlakani," Choo Khyung-ho amewaambia waandishi wa habari. Hata hivyo, ameongeza kwamba alimwomba Yoon Suk-yeol kuondoka katika chama. PPP "haitetei sheria ya kijeshi ya rais iliyo kinyume na katiba," amesema.
Uthibitisho wa lazima kutoka kwa Mahakama ya Katiba katika tukio la kuondolewa mamlakani
Ikiwa hoja hiyo itapitishwa, Yoon atasimamishwa kazi akisubiri uthibitisho wa kutimuliwa kwake na Mahakama ya Kikatiba. Ikiwa majaji wataidhinisha hilo, ataondoka mamlakani na uchaguzi mpya wa urais utalazimika kufanyika ndani ya siku 60. Chama cha Kidemokrasia, kikosi kikuu cha upinzani, pia kmetangaza kuwasilisha malalamiko dhidi ya rais kwa "uasi", uhalifu ambao kinadharia unaadhibiwa na kifo (ambao haujatumiwa nchini Korea Kusini tangu mwaka 1997).
Yoon Suk-yeol hajaonekana hadharani tangu hotuba yake ya mwisho kwenye televisheni ya taifa, alfajiri ya Jumatano, kutangaza kuondolewa kwa sheria ya kijeshi ambayo alikuwa ametangaza jioni ya siku iliyotangulia.
Ofisi yake imetangaza kujiuzulu kwa Waziri wa Ulinzi Kim Yong-hyun siku ya Alhamisi. Lakini wengine walio karibu na rais, akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani Lee Sang-min, wanasalia katika nyadhifa zao.
Sheria ya kijeshi ilianzishwa mara ya mwisho mwaka 1980 nchini Korea Kusini, wakati mamia ya maelfu ya watu waliingia mitaani kupinga mapinduzi ya kijeshi. Ukandamizaji ulisababisha vifo vya mamia ya watu.
Hatua ya Yoon Suk-yeol iliwashangaza washirika wa Korea Kusini, kwanza kabisa Marekani, ambayo ina takriban wanajeshi 30,000 nchini humo. Washington imesema ilipata taarifa kuhusu tangazo la sheria ya kijeshi kutoka kwa televisheni.