Majaliwa: Rais Samia Ameimarisha Amani Kupitia 4R, na Ameongoza kwa mafanikio

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amepongeza juhudi na uongozi bora wa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, katika kupeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuliongoza taifa kwa mafanikio makubwa.

Akizungumza siku ya Jumapili, Januari 19, 2025, mkoani Dodoma, wakati wa siku ya pili ya Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, Majaliwa amewapongeza viongozi hao kwa uvumilivu, busara, haki, weledi, na ukomavu wa kiuongozi, ambao umekuwa chachu ya maendeleo na matumaini mapya kwa Watanzania.

Majaliwa ameeleza kuwa mafanikio ya Rais Samia yamevuka mipaka ya taifa na kutambuliwa kimataifa, akitaja mifano ya shahada za heshima za udaktari wa falsafa alizotunukiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Tanzania), Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru (India), na Chuo Kikuu cha Ankara (Uturuki). Pia, amekumbusha jinsi jarida maarufu la Forbes lilivyomtangaza Rais Samia kuwa mwanamke wa pili shupavu barani Afrika mwenye ushawishi mkubwa, mara tatu mfululizo.

“Heshima hii si tu inathibitisha kazi nzuri ya Rais wetu ndani ya taifa, lakini pia inaonyesha jinsi Tanzania inavyozidi kuheshimiwa kimataifa kutokana na uongozi wake wa kipekee,” amesema Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu ameeleza jinsi falsafa ya Rais Samia ya “4R”—maridhiano, ustahimilivu, mageuzi, na ujenzi wa taifa-imeimarisha umoja, mshikamano, na uhusiano wa kikanda na kimataifa. Vilevile, amempongeza Rais Mwinyi kwa mchango wake mkubwa wa kuimarisha amani na maendeleo visiwani Zanzibar kupitia uongozi wake kama Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii