Moto wa nyika unaowaka kwa kasi katika sehemu za Los Angeles, Marekani, umeharibu majengo na kusababisha msongamano wa magari huku zaidi ya watu 30,000 wakihamishwa.
Maafisa wanasema, takribani ekari 2,921 (hekta 1,182) za eneo la Pacific Palisades kati ya miji ya pwani wa Santa Monica na Malibu zimeteketezwa na moto, na wameonya juu ya hatari ya moto kuenea kutokana na upepo kufuatia hali ya hewa ya ukame.
Afisa mmoja wa zimamoto alikiambia kituo cha runinga cha KTLA, kuwa watu kadhaa wamejeruhiwa, wengine wakiwa wameungua usoni na mikononi. Afisa huyo aliongeza kuwa zima moto mmoja wa kike amepata jeraha la kichwa.
Moto wa pili ulizuka takriban maili 30 (kilomita 50) karibu na Pasadena na kuunguza takribani ekari 400 (hekta 162) katika saa chache, kulingana na Cal Fire.
Maafisa wa zima moto wanasema moto wa tatu ulianza huko Sylmar, katika Bonde la San Fernando kaskazini-magharibi mwa Los Angeles, na kusababisha wakazi kuhamishwa.
Mkuu wa Zimamoto wa Los Angeles, Kristin Crowley amesema katika mkutano wa waandishi wa habari kwamba zaidi ya watu 30,000 na nyumba 10,000 zimeathiriwa.