Atolewa Uvimbe Wenye Uzito wa Kilo 5.5 Kwenye Mfuko wa Mayai

Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 52 (jina limehifadhiwa) mkazi wa Bagamoyo mkoani Pwani, Januari 7, 2025 amefanyiwa upasuaji mkubwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, katika mfuko wa mayai wa upande wa kushoto, huku madaktari wakifanikiwa kutoa uvimbe wenye uzito wa kilogramu 5.5.

Upasuaji huo umeongozwa na jopo la wataalamu na madaktari wa Hospitali ya Rufaa Mwananyamala, likiongozwa na Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake Dkt. Taiba Kassim Haidar, Dkt. Onesmo Laizer na Dkt. Luponya Shelembi, Mtaalamu wa dawa za ganzi Meshack Hinyuka na Kelvin Mapunda, pamoja na Wauguzi ambao ni Godfrey Lukenge na Ernest Hekela.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi Dkt. Taiba Kassim Haidar amesema zoezi la upasuaji limeenda vizuri na sasa uvimbe huo wenye kulogramu 5.5 umepelekwa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi.

“Alikuja tangu mwezi wa nane hapa hospitali baada ya kuangaika kwa muda mrefu, tukawa tunaendelea kumungalia kwa ukaribu hatimaye leo tumefanikiwa kumfanyia oparesheni katika mfuko wa yai la kushoto na kutoa uvimbe huo na anaendelea vizuri kabisa”. Amesema Dkt. Taiba.

Kwa upande wake mtoto wa mwanamke huyo Yahya Miraji ameishukuru timu ya wataalamu waliosaidia kukamilika kwa upasuaji huo kutokana na wakati mgumu aliokuwa anapitia mama yake.

“Kiukweli nashukuru sana kwa madaktari wote na wataalamu ambao wameshiriki zoezi hilo, kwa sababu mama tumbo lilikuwa linamuuma sana na alikuwa hawezi kulala vizuri”.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii