Mwamba Ajaza Mchanga Magunia 115 Kuwatapeli Wakulima wa Mahindi

Wananchi wa Palangawanu, halmashauri ya wilaya ya Wanging'ombe, mkoani Njombe, wamekumbwa na huzuni baada ya kubaini kuwa wametapeliwa fedha zao za mahindi

Katika godauni lililokuwa na mahindi, walikuta magunia ya mchanga, huku mahindi yakiwa yameuzwa na msimamizi wa godauni, Robart Matimbwa (31).

Mkuu wa wilaya ya Wanging'ombe, Zacharia Mwansasu, amefika katika godauni hilo na kugundua shehena ya magunia ya mchanga yakiwa yamepangwa pamoja na magunia ya mahindi. Amesisitiza kwa wananchi waache kuaminiana kwa mali kauli katika biashara, hali inayowapelekea kutapeliwa zaidi ya milioni 66, bila kuwa na vielelezo vyovyote vinavyothibitisha makubaliano yao na Robart.


“Hakuna mali kauli. Leo hii mnadai fedha zaidi ya milioni 66 ambazo mmetapeliwa kwa mali kauli tu, lakini hamna kielelezo chochote. Robert sio mzaliwa wa Palangawanu; amekuja kama mfanyabiashara yeyote. Natoa angalizo: akija mfanyabiashara yeyote, hata kama amekutamanisha kwa bei, usikimbilie bei. Kimbilia kwanza usalama wa mzigo wako,” amesema DC Mwansasu.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, amethibitisha kuwa tayari wanamshikilia Matimbwa, ambaye alikuwa na jukumu la kusimamia godauni lililomilikiwa na Frank Nyange (41) wa Dar es Salaam.


"Alipewa kusimamia godauni hili, ambapo kulikuwa na magunia 2063 ya mahindi. Baada ya upekuzi, imebainika kwamba kulikuwa na gunia 610 za mahindi na 115 za mchanga. Magunia mengine yameuzwa na kijana huyu. Tunamshikilia kwa tuhuma hizo.


Kijana huyu alijizolea umaarufu na kupata wakulima wengine ambao walimwamini na kumpatia debe 6335 za mahindi, zenye thamani ya milioni 63. 35, ambazo zilikuwa mali kauli. Alipokuwa anajaribu kuziuza Dar es Salaam, alidai fedha hizo bado hajarejeshewa,” amesema Kamanda Banga.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii