Zaidi ya vijana 500 wa kiafrika wakutana Arusha kuzungumzia umiliki wa ardhi

Zaidi ya vijana 500 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Jumatatu wamekutana Jijini Arusha ,Tanzania  kujadili namna watakavyoweza  kupata fursa na haki ya kumiliki ardhi katika  nchi  zao, na kuitumia kujikwamua kwenye umaskini. 

Mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya kimataifa inayofuatilia haki za vijana katika masuala ya ardhi kwa ushirikiano na umoja wa Afrika (AU) na shirika la maendeleo la ujerumani (GIZ), unalenga kuwakutanisha pamoja vijana na wadau wengine wakiwemo viongozi wa serikali na taasisi za kiraia, ili kujadili namna ya kuwezeja vijana kufahamu umuhimu wa ardhi, na namna ya kuitumia kujikwamua kimaisha.

Wakizungumza katika mkutano huo unaofanyika wakati ambao asilimia kubwa ya vijana wa nchi za bara la Afrika wanategemea kupata ardhi kwa kurithi baada ya wazazi wao kufariki , baadhi ya vijana walisema kuwa wakati umefika wa serikali za Afrika kuweka sheria na sera rafiki zinazotekelezeka na zenye tija kwa vijana.

Mkutano huo pia ulileta pamoja wataalam wa ardhi kutoka serikali za baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Tanzania ambao walisema kwamba kuna haja kubwa ya kuongeza nguvu kuwawezesha vijana kuelewa umuhimu wa ardhi na namna inavyoweza kuwasaidia katika harakati za kukabiliana na hali ya umasikini .

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii