Mwanachuo ashtakiwa kuchapisha habari potovu kuhusu ‘jeneza la Ruto’

MWANAFUNZI wa chuo kikuu cha Moi ameshtakiwa kwa kuchapisha habari za uwongo kumhusu Rais William Ruto.

David Ooga Mokaya, aliye mwaka wa nne katika chuo hicho alifikishwa kortini Jumatatu, Novemba 18, 2024, alasiri na kushtakiwa kwa kutumia mtandao wake wa X-Space vibaya.

Hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi, alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Virginia Kariuki kwamba Mokaya “alichapisha habari za uwongo kuhusu msafara wa idara ya kijeshi ukiwa na jeneza iliyofunikwa bendera ya Kenya ikiwa na mwili wa Rais Ruto.”

Katika cheti cha mashtaka, Mokaya alidaiwa alichapisha habari hizo za kupotosha msafara huo ukitoka chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee.

Hakimu alielezwa Mokaya alichapisha habari hizo katika mtandao wake wa “X Space Account” almaarufu – “Landlord@bozgabi”.

Mahakama ilielezwa na Bi Kariuki kwamba lengo la Mokaya lilikuwa la kuaminisha umma kwamba habari hizo ni za kweli.

Mokaya alikana shtaka hilo kisha akaomba aachiliwe kwa dhamana.

Kupitia kwa wakili wake, mwanafunzi huyo alisema anatazamia kuhitimu katika somo la Uchumi na Fedha Desemba 2024.

Hakimu alielezwa Mokaya alitiwa nguvuni na maafisa wa polisi jijini Eldoret na kusafirishwa hadi jijini Nairobi.

Korti iliambiwa mshtakiwa alichapisha habari hizo mnamo Novemba 13, 2024 mahala pasipojulikana katika jamhuri ya Kenya.

Inadaiwa kuwa madhumuni ya mshtakiwa yalikuwa kudanganya umma ikitiliwa maanani jeneza hilo lilikuwa limefunikwa kwa bendera ya Kenya na kusikindikizwa na maafisa wa kijeshi wakiwa wamejikwatua mavazi rasmi ya sherehe.

Mahakama iliombwa imwachilie mshtakiwa kwa dhamana akakamilishe mtihani wake na kujiandaa kuhitimu.

Hakimu aliambiwa mshtakiwa hatatoroka ila atafika kortini wakati wa kusikizwa kwa kesi na wakati wowote ule atakapotakikana.

Hakimu alielezwa atilie maanani kwamba mshtakiwa ni mwanafunzi na kamwe hawezi kupata kiwango cha juu cha dhamana.

Pia wakili wa mshtakiwa alisema dhamana ni haki ya kila mshukiwa.

Bi Kariuki hakupinga ombi la dhamana la mshtakiwa ila aliomba korti imwonye asivuruge mashahidi.

Akitoa uamuzi Bw Ekhubi alisema dhamana ni haki ya mshtakiwa na akamwachilia kwa dhamana ya Sh100,000 na mdhamini mmoja ama dhamana ya pesa tasilimu Sh50,000.

Kesi hiyo itatajwa Novemba 21 kwa maagizo zaidi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii