Ukraine inasema wanajeshi wake hawatowahi kujisalimisha kwa Urusi, kauli hii inakuja wakati huu ikiwa ni siku Elfu moja tangu Moscow kuanzisha uvamizi wake.
Katika hatua nyengine, Kremlin na yenyewe imeahidi kupata ushindi pamoja na kuzidisha tishio lake la kutumia silaha za nyukilia.
Maadhimisho haya ya miaka Elfu moja ya mapigano yamekuja wakati huu Urusi ikitekeleza shambulio katika mji wa Sumy nchini Ukraine, watu tisa wakiripotiwa kuuawa akiwemo mtoto.
Rais Volodymyr Zelensky amechapisha picha za maofisa wa idara ya uokoaji wakitoa miili ya watu kwenye majengo yalioharibiwa, akitoa wito kwa mataifa washirika wa Kyiv kuishinikiza Urusi kuachana na vita.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Ukraine nayo pia imezitaka nchi washirika wake kuipa nchi yake msaada wa kijeshi unaohitajika ilikuweza kumaliza vita.
Wizara hiyo ya mambo ya kigeni imesema Ukraine haitowahi kujisalimisha na kwamba jeshi la Urusi litawajibishwa kwa kukiuka sheria za kimataifa.Kremlin kwa upande wake imeahidi kupata ushindi dhidi ya Ukraine.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov katika taarifa yake amesisitiza kwamba oparesheni dhidi ya Ukraine zitaendelea na zitamalizika.
Matamshi ya Peskov yamekuja wakati huu pia rais Putin akiwa ametia saini amri inayoongeza wigo wa wakati gani #moscow inaweza kutumia silaha za nyuklia, uamuzi huu ukituma ujumbe wa moja kwa moja kwa nchi za Magharibi na #ukraine.