Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imehitimisha ziara ya kukagua miradi katika sekta ndogo ya ufugaji nyuki kwa kuipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa usimamizi mzuri huku ikitambua mchango mkubwa wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta hiyo ndogo.
Hayo yamesemwa na wajumbe wa Kamati hiyo kwa nyakati tofauti leo Novemba 13, 2024, walipotembelea kiwanda cha kuchakata lita 2,000 kwa siku kilichopo Nzega Tabora kilichojengwa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mfuko wa Misitu (Taff).
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Timotheo Mzava na Makamu wake Najma Guga walionesha kuridhishwa na miradi yote waliyoitembelea.
“Miradi ya sekta ndogo ya nyuki tumeridhishwa imekwenda vyema lakini pia unapotembelea miradi hii yote jambo moja linajitokeza ni kuwa chini ya Rais Samia na uongozi wa Wizara mageuzi makubwa na utashi wa kuiboresha sekta hii unaonekaa wazi,” alisema Mzava.
Aidha, wakiwa njiani mkoani Singida Kamati hiyo ilipata fursa ya kutembelea mradi mkubwa wa sekta binafsi wa Kijiji cha Nyuki unaozalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo asali, nta na kuuza ndani na nje ya nchi.