Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Manispaa ya Kinondoni leo imetoa taarifa miezi mitatu katika kupambana na vitendo vya rushwa ikitaja idadi ya watoto wanaobakwa na kulawitiwa kwa siku pamoja uhalifu mwingine wa masuala ya rushwa na kuahidi kukomesha uhalifu huo.
Kaimu Mkuu wa Takukuru Manispaa ya Kinondoni, Christian Nyakizee ametaja idadi ya watoto wanaobakwa na kulawitiwa kwa siku jambo linaloonesha kuporomoka kwa maadili na kuahidi kukomesha vitendo hivyo.
Nyakizee amesema hayo wakati akizungumza na wanahabari juu ya warsha walizofanya na maofisa wa polisi dawati la jinsia pamoja na maofisa wa ustawi wa jamii juu ya kukomesha matendo hayo.
Aidha Nyakizee amesema Agosti 30 mwaka huu walitoa mafunzo ya kuzuia uhalifu huo na maofisa wa ustawi wa jamii 25 kutoka Kata za Manispaa ya Kinondoni kwenye Ukumbi wa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni.
Mafunzo ya maofisa ustawi wa jamii ilifuatiwa mafunzo kwa maofisa wa polisi iliyofanyika Ukumbi wa Mikutano wa ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Septemba 26 mwaka huu.
Nyakizee ameendelea kusema mafunzo hayo yalihudhuriwa na askari polisi 37 kutoka katika madawati na jinsia 14 kutoka Manispaa ya Kinondoni ikiwemo, Kituo cha Oysterbay, Kijitonyama, Chuo Kikuu UDSM, Magomeni, Urafiki, Mburahati, Gogoni, Magufuli Bus Terminal, Mavurunza, Kawe, Mabwepande, Goba na Madale.
Katika Warsha hiyo ilibainika kuwa katika Manispaa ya Kinondoni kwa kipindi cha Julai mwaka huu watoto 36 walibakwa na kulawitiwa na Agosti mwaka watoto 29 walibakwa na kulawitiwa. Alisema Nyakizee.