Taifa hilo la kusini mwa Afrika limekuwa likishuhudia machafuko tangu tarehe tisa ya mwezi Oktoba, wakati chama tawala cha Frelimo ambacho kimekuwa madarakani kwa kipindi cha miaka 50 kupata tena ushindi katika uchaguzi wa urais.
Kinara wa upinzani Venancio Mondlane, ambaye alisema matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa yamekarabatiwa, alijitangaza mshindi.
Venancio aliitisha maandamano hayo makubwa akisema kwamba yalikuwa ni muhimu kwa mustakabali wa taifa kwa sasa.
Mondlane mwenye umri wa miaka 50 na mtangazaji wa zamani wa radio ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hawezi kutoa taarifa kuhusu alipo.
Maelfu ya watu wameshirki maandamano hayo, polisi wakitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya. Mji huo wenye idadi ya zaidi ya watu milioni moja umesalia mahame, maduka yakifungwa sawa na shule, vyuo vikuu na benki.
Akitumia mitandao ya kijamii, Mondlane amewataka wafuasi wake kushiriki maandamano hayo ambayo yamegeuka kuwa machafuko, makabiliano makali baina yao na polisi yakishuhudiwa.
Karibia watu 18 wameuwa katika machafuko ya baada ya uchaguzi kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW.)
Katika upande mwengine shirika lisilo la kiserikali la ndani la Centre for Democracy and Human Rights (CDD) limeripoti kuuawa kwa watu 24.
Afisa wa polisi naye pia aliuawa katika maandamano ya wikendi iliopita kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa ulinzi Cristovao Chume siku ya Jumanne.