Wafanyakazi wa viwanja vya ndege nchini Kenya wameamua kusitisha mgomo na kurudi kazini baada ya kufikia makubaliano na serikali.
Katika makubaliano hayo ya kurudi kazini kwa wafanyakazi hao, serikali itaruhusu uchunguzi wa stakhabadhi kuhusu ukodishaji wa miaka 30 wa uwanja wa ndege wa JKIA na kampuni ya India ya Adani.
Vyama vya wafanyakazi kwenye viwanja vya ndege vya JKIA pamoja na vile vya Mombasa na serikali kufuatia mkutano kati ya Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir, Viongozi wa Muungano wa wafanyakazi na katibu wa Muungano wa wafanyakazi nchini Kenya Cotu Francis Atwoli.
Waziri wa Uchukuzi Chirchir ameahidi kwamba mkataba ulioafikiwa kati ya serikali na kampuni ya Adani utawasilishwa mahakamani ambapo serikali imeshtakiwa ili kuruhusu uchunguzi wa wazi.
Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli amesema kwamba serikali imekubali kuanzisha mazungumzo ya mishahara na wafanyakazi mbali na makubaliano mapya ya majadiliano katika kipindi cha miezi miwili.
"Waliamua kuwapatia wafanyakazi hao wa viwanja vya ndege siku 10 kuchunguza stakhabadhi hizo za Adani kabla ya mkutano mwengine kufanywa na washikadau" , amesema Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli.
Hii ina maana kwamba operesheni za kawaida sasa zitarudi katika viwanja vya ndege vya JKIA pamoja na vile vya Mombasa, Kisumu na Eldoret baada ya huduma kulemazwa huku baadhi ya mashirika ya ndege yakipata hasara kubwa.