Bangi Aina ya Skanka KILO 1,815 Yakamatwa

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata kilogramu 1,815 za dawa

za kulevya aina ya skanka katika oparesheni iliyofanyika August 28, 2024 hadi September 02, 2024 katika maeneo ya Luguruni Mbezi na Magomeni Jijini Dar es salaam ambapo Watuhumiwa watano wamekamtwa kuhusiana na dawa hizo.


Akiongea Jijini Dar es salaam leo September 09,2024, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo amesema “Watuhumiwa waliokamatwa wanatambulika kwa majina ya Richard Henry Mwanri (47) ambaye ni Mfanyabiashara na Mkazi wa Mbezi Makonde Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam na Felista Henry

Mwanri (70) Mkulima na Mkazi wa Luguluni Mbezi Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam ambaye ni Mmiliki wa nyumba zilipokutwa dawa hizo za kulevya.


“Watuhumiwa wengine ni Athumani Koja Mohamed (58) Mfanyabiashara, na Mkazi wa Tanga, Omary

Chande Mohamed (32) Dereva bajaji na Mkazi wa Buza Jijini Dar es Salaam na Juma Abdallah Chapa (36) Mkazi wa Kiwalani jijini Dar es Salaam, aidha katika operesheni hiyo, gari aina ya Mitsubishi Pajero lenye namba za usajili T 551 CAB na bajaji yenye namba za usajili MC 844 CZV vilikamatwa”


“Richard Mwanri ni Mhalifu ambaye amekuwa akipokea dawa za kulevya kutoka Nchi mbalimbali na kuziingiza nchini kwa usafiri wa magari zikiwa zimefichwa kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine kisha kusambazwa kwa wauzaji wengine katika maeneo mbalimbali Nchini”


Kwa siku za hivi karibuni, dawa za kulevya aina ya skanka zimekuwa zikikamatwa mara kwa mara Nchini, skanka ni aina ya bangi ya kusindika yenye kiwango kikubwa cha kemikali yenye sumu aina ya Tetrahydrocannabinol (THC) ambayo inaweza kuharibu mfumo wa fahamu, akili na kusababisha magonjwa yasiyoambukiza kama vile moyo, figo, na ini. Matumizi ya skanka kwa wajawazito yanaweza kusababisha madhara kwa mtoto aliye tumboni ikiwemo kuathiri maendeleo ya ubongo na kuzaliwa na uzito mdogo.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii