Serikali Yaondoa Sharti la Kusoma Law School

Bunge limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Shule ya Sheria Tanzania wa Mwaka 2024 ambao umeondoa sharti la kila mhitimu wa shahada ya sheria kupita katika shule hiyo.


Sharti hilo lilimtaka kila mhitimu wa shahada ya sheria nchini kulazimika kupitia na kufaulu masomo ya sheria kwa vitendo hata kama hakusudii kufanya kazi za uanasheria katika utumishi wa umma.


Baada ya kuwasilishwa muswada huo bungeni Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, wabunge walichangia na kisha kuridhia. Profesa Kabudi alisema muswada huo ulilenga kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizobainika katika utekelezaji wa masharti ya sheria hiyo.


Alisema umelenga kuondoa sharti la kila mhitimu wa shahada ya sheria kulazimika kupitia na kufaulu masomo ya sheria kwa vitendo hata kama hana mpango kufanya kazi za kisheria katika utumishi wa umma. Lengo lingine ni kuongeza wigo wa shule kutoa mafunzo ya kozi nyingine maalumu za mafunzo ya sheria kwa vitendo.


Muswada huo una sehemu mbili, mojawapo ikihusisha masharti ya utangulizi yanayojumuisha jina la muswada na namna masharti yanavyopendekezwa kurekebishwa na nyingine ni marekebisho katika vifungu mbalimbali vya sheria.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii