Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua awasilisha kesi mahakamani

Naibu wa Rais wa Kenya aliyetimuliwa Rigathi Gachagua amefika mahakamani kupinga mchakato wa kuondolewa wake Ofisini na bunge.


Kupitia Wakili wake Paul Muite, Gachagua pia ameitaka mahakama kutoa maagizo yanayomuzuia Rais William Ruto kumpendekeza mrithi wake hadi pale ambapo kesi yake itakaposikilizwa.

Gachagua amepinga mchakato wote uliopelekea kutimuliwa kwake kwa madai kwamba makosa anayokabiliwa nayo hayana msingi na kwamba ushahidi uliowasilishwa dhidi yake ulikuwa hafifu.

Anaeleza kwamba bunge la Seneti lilishtahili kutoegemea upande wowote wakati wa kuamua mswada wa kutimuliwa kwake.

Adiha anasisitiza kwamba ushahidi uliotumika katika kesi ya kutimuliwa kwake haukustahili na haukuafikia vigezo kwa mujibu wa sheria.

Vilevile ametaka bunge la kitaifa kuzuiliwa kujadili kuhusu mrithi wake ambaye amependekezwa na Rais Ruto.

Tayari pendekezo la Rais William Ruto, Waziri wa usalama wa ndani Professa Kithure Kindiki ameidhinishwa na bunge la kitaifa kuchukua nafasi ya Rigathi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii