ICC: Mwendesha mashtaka aamuru 'kuanzishwa upya' kwa uchunguzi nchini DRC

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa siku ya Jumatatu Oktoba 14, mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ametangaza "kuanzisha upya" uchunguzi wake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Uamuzi huu unafuatia ziara ya Naibu Waziri wa Sheria wa Kongo, Samuel Mbemba Kabuya, huko Hague, wiki iliyopita.


Uchunguzi mpya nchini DRC uliotangazwa Jumatatu Oktoba 14 na Karim Khan, mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), utazingatia uhalifu wa kivita uliofanywa tangu mwezi Januari 2022 katika mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Kongo. Kulingana na taarifa yake kwa vyombo vya habari, wahusika wote wa uhalifu watalengwa.

Tangu mwaka 2004, maafisa saba wa Kongo tayari wamepewa hati za kukamatwa kutoka ICC - na watano kati yao wamehukumiwa - kama sehemu ya uchunguzi wa uhalifu uliofanyika nchini humo.

Karim Khan pia anabainisha kwamba anataka kupendelea "mbinu ya njia mbili" na, kwa upande mmoja, uchunguzi wenyewe na, kwa upande mwingine, kuunga mkono vyombo vya sheria vya Kongo. Kuhusiana na hilo, amechukua fursa hiyo pia kukaribisha kuundwa kwa kamati ya uongozi itakayoshughulikia uanzishwaji wa Mahakama Maalum ya Jinai kwa DRC.

Hali katika Kivu Kaskazini "ilihusishwa na mifumo ya mara kwa mara ya vurugu na uhasama"

Moja ya vipengele vya sera ya jinai ya Karim Khan inalenga kuunga mkono mataifa ili kutoa - kadri inavyowezekana - haki katika ardhi yao. Nchini DRC, mkataba wa aina hii ulitiwa saini na serikali mwezi Juni 2023, mwezi mmoja baada ya serikali ya Kinshasa kuitaka ICC kuchunguza tena katika ardhi yake.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Karim Khan pia inabainisha kwamba, kwake, matukio ya hivi punde ya vurugu huko Kivu Kaskazini, ninanukuu, "yanahusishwa na mifumo ya mara kwa mara ya vurugu na uhasama ambao umekuwa ukikumba eneo hilo" kwa zaidi ya miaka 20 . Tangu kufunguliwa kwa uchunguzi wa ICC kuhusu uhalifu uliofanyika DRC mwaka 2004, maafisa saba wa Kongo tayari wamepewa hati za kukamatwa na taasisi hiyo - na watano kati yao wamehukumiwa, akiwemo Jean- Pierre Bemba, Thomas Lubanga na Bosco Ntaganda.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii