William Ruto Aashiria Sababu ya Kususia Ibada ya Embu Iliyohudhuriwa na Gachagua

WAKAZI wa Mlima Kenya sasa wameonekana kumkataa Rais William Ruto kwa kukosa kumnusuru naibu wake Rigathi Gachagua anayekabiliwa na hatari ya kutimuliwa afisini na maseneta wiki hii.

Aidha, wamekuwa wakiwazomea hadharani wabunge waliopitisha hoja ya kumtimua Gachagua afisini katika Bunge la Kitaifa Jumanne wiki iliyopita.

Ili kujiepusha na hasira za wakazi hao, Rais Ruto Jumamosi jioni alifutilia mbali ziara yake katika kaunti ya Embu ambako Jumapili aliratibiwa kuhudhuria maadhimisho ya miaka 34 tangu kuanzishwa kwa dayosisi ya Embu ya Kanisa la Kianglikana Nchini (ACK).

Awali, Mbunge wa Manyatta Gitanga Mukunji alikuwa amethibitisha kuwa Dkt Ruto alipaswa kuwa mgeni wa heshima katika sherehe hiyo katika Chuo cha Mafunzo ya Walimu cha Kigari, kilichoko eneo bunge lake.

“Hii sherehe inafanyika katika eneo bunge langu. Rais ndiye mgeni mheshimiwa. Endapo hatafika, bila shaka atawakilishwa na naibu wake,” Bw Mukunji alisema

Jana, Rais Ruto alifichua mbele ya waumini wa Kanisa la AIC Milimani, Nairobi, kwamba hakuwa amepanga kuungana nao kwa ibada ya Jumapili bali aliratibiwa kuhudhuria kwingineko.

“Nilikuwa nimeratibu kwenda kwingine. Ilinilazimu kujadiliana na watu maeneo mengine kwa sababu sikutaka kukosa sherehe hii,” Rais Ruto akasema.

Ibada hiyo iliandaliwa mahsusi kuadhaminisha miaka 30 tangu kujengwa kwa kanisa hilo la AIC Milimani.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii