Maafisa tisa wa utawala uliopinduliwa 'wavuliwa' uraia wao kwa muda

Maafisa tisa wa utawala wa kiraia wa Niger uliopinduliwa mnamo Julai 2023 "wamevuliwa" uraia wao, baada ya kushukiwa haswa "ujasusi kwa mataifa ya kigeni" na "njama dhidi ya mamlaka ya serikali", serikali ya kijeshi imetangaza.


Jenerali Abdourahamane Tiani, Mkuu wa Nchi, "meitia saini Alhamisi, Oktoba 10, agizo la kuwavua uraia baadhi ya watu kwa makosa mbalimbali waliofanya na kuadhibiwa kisheria," serikali imesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Miongoni mwa watu hao tisa "waliovuliwa uraia wa Niger" ni majenerali Mahamadou Abou Tarka, wa Mamlaka ya Juu ya Kudumisha Amani, na Karingama Wali Ibrahim, mkuu wa zamani wa kikosi cha walinzi wa rais.

Daouda Djibo Takoubakoye, naibu mkurugenzi katika ofisi ya rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum, pamoja na mshauri wake wa usalama, Rhissa Ag Boula, pia ni miongoni mwa watu hao, pamoja na washauri wa katika ofisi ya rais.

Watu hao tisa "wanashukiwa hasa" kwa "kufanya shughuli zinazoweza kuvuruga amani na usalama wa umma" na "ujasusi kwa nchi za kigeni kwa nia ya kuchochea uhasama dhidi ya serikali" au " kuwezesha kuingia kwa majeshi ya nchi za kigeni katika eneo la Niger,” inaeleza serikali.

Pia "wanashukiwa" kwa "kushiriki katika biashara ya kudhoofisha jeshi" na "usambazaji wa data au maoni ambayo yanaweza kuvuruga utulivu wa umma", serikali inaongeza.

Serikali inasema inafanya kazi kwa mujibu wa sheria iliyotiwa saini mwishoni mwa mwezi Agosti iliyoruhusu kuundwa kwa faili la watu au taasisi "zinazohusika katika vitendo vya kigaidi au makosa yoyote yanayoathiri kimkakati na/au maslahi ya kimsingi ya taifa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii