Wanne wa Kampuni ya Mikopo ya OYA Watuhumiwa Kuua Wakati Wakidai Marejesho

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za mauaji ya Juma Said Mfaume, Miaka 40, Mfanyabiashara na mkazi wa Mbagala Mlandizi.


Inadaiwa kuwa tarehe 7/10/2024 katika kitongoji cha Mbagala, Wilaya ya Kipolisi Mlandizi, Mkoa wa Pwani watu wanne ambao ni wafanyakazi wa kampuni ya mikopo ya OYA walifika nyumbani hapo kwa lengo la kudai fedha za marejesho ya mkopo kwa mke wa Juma Said Mfaume aitwaye Khadija Ramadhani,

Baada ya kufika nyumbani kwa Juma Mfaume aliwaeleza kuwa mkewe hayupo lakini watuhumiwa hao walilazimisha kuingia ndani kwa nguvu huku wakimshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia fimbo na baadaye alianguka chini na kupoteza fahamu.

Kutokana na hali hiyo watuhumiwa walimbeba Juma Mfaume kwa kutumia gari lao ili wampeleke hospitali na alifariki akiwa anapatiwa matibabu katika kituo cha Afya cha Mlandizi.


Mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na daktari kisha kukabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linatoa wito kwa makampuni na taasisi za kifedha kufuata taratibu za kisheria katika kudai fedha kutoka kwa wateja wao ili kuepusha usumbufu na madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo uharibifu wa mali, kujeruhi na vifo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii