Mwanasiasa wa upinzani nchini Ufaransa Marine Le Pen, ambaye alikuwa kiongozi wa muda mrefu wa chama cha siasa za mrengo wa Kulia, National Rally, amefunguliwa mashtaka jijini Paris, kwa madai ya matumizi mabaya ya fedha za bunge la Umoja wa Ulaya.
Mgombea huyo wa zamani wa urais pamoja na wanachama zaidi ya 20 wa chama chake, pia wanakabiliwa na mashtaka hayo.
Wanadaiwa kuwaajiri wafanyakazi waliokuwa wanafanya kazi za chama na badala ya bunge la Umoja wa Ulaya na kutumia fedha za bunge hilo kuwalipa mshahara kati yam waka 2004 hadi 2016.
Hata hivyo, kupitia msemaji wake wa chama Laurent Jacobelli, Le Pen amekanusha madai hayo, na kuongeza kuwa watathibitisha Mahakamani kuwa fedha za Umoja wa Ulaya, hazikutumiwa kuwalipa wafanyakazi wa chama.
Viongozi wa mashtaka wanataka chama hicho kirejeshe Euro Milioni 3 na tayari imerejesha Euro Milioni 1, lakini chama cha Le Pen kinasema hatua hiyo, haimaanishi kuwa inakiri kutenda kosa hilo.
Iwapo Le Pen, akipatikana na hatia hiyo baada ya kesi hiyo itakayoendelea kwa miezi miwili, atafungwa jela na kulipa faini, na pia kuzuiwa kuwania nyadhifa yoyote ya kisiasa kwa miaka 10, hali ambayo inaweza ikaathiri mipango yake ya kuwania urais katika miaka ijayo.