WAZIRI wa Kawi na Mafuta Opiyo Wandayi amepuuzilia mbali ripoti kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) ulikumbwa na uhaba wa mafuta ya ndege, hali iliyochelewesha safari za ndege.
Akiongea alipotembelea kiwanda cha kusafisha mafuta cha Kenya Petroleum Refineries Ltd Mombasa, Bw Wandayi alisema shida hiyo ilisababishwa na tatizo katika pampu ya mafuta katika JKIA.
Kulingana na Waziri huyo, hitilafu hiyo ilisuluhishwa ndani ya muda wa saa moja na nusu kisha hali ya kawaida ikarejelewa katika uwanja huo wenye shughuli nyingi zaidi nchini.
Bw Wandayi alieleza kuwa chini ya mpango mpya wa ununuzi wa mafuta kati ya Kenya na Serikali ya Muungano wa Milki ya Kiarabu (UAE) uliofikiwa 2023, Kenya haiwezi kukumbwa na ukosefu wa aina yoyote ya mafuta.
“Kulitokea hitilafu kidogo tu Alhamisi asubuhi, kasoro kwenye pampu ya kupitisha mafuta na sio kwamba kuna uhaba wa mafuta,” Bw Wandayi akaeleza.
“Hatutashuhudia shida ya ukosefu wa mafuta kwani chini ya mkataba kati ya serikali ya Kenya na ile ya UAE mikakati imewekwa kuhakikisha kuwa uwepo wa aina mbalimbali za mafuta ya kutosheleza mahitaji ya kitaifa,” akaeleza.
Bw Wandayi pia alisema serikali inaendesha mpango wa kuunganisha kampuni ya Kenya Petroleum Refineries Ltd na ile ya Kenya Pipeline Corporation kuimarisha usambazaji wa mafuta nchini.
Kauli ya Waziri huyo ilijiri saa kadhaa baada ya Mamlaka ya Kusimamia Viwanja Vya Ndege Nchini (KAA) kukubali kwamba kulishuhudiwa ukosefu wa mafuta katika uwanja wa JKIA hali iliyoathiri safari za ndege.
Kwenye taarifa, mamlaka hiyo ilieleza kuwa tatizo hilo lilisuluhishwa haraka na shughuli za kawaida zikarejelewa katika uwanja huo.
Changamoto hiyo ilisababisha wasiwasi miongoni mwa wasafiri huku baadhi yao wakilalamika baada ya safari zao kucheleweshwa.