Kamala Harris aahidi kuinga mkono Ukraine katika vita dhidi ya Russia

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris Alhamisi aliahidi msaada kwa Ukraine, akimuzungumzia mpinzani wake Donald Trump bila kumtaja jina, akisema wale ambao wanataka Ukraine ibadilishe ardhi yake kwa ajili ya amani na Russia, wanaunga mkono “mapendekezo ya kujisalimisha.”

Harris, mgombea urais wa chama cha Democratic, alizungumza akiwa pamoja na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kwenye White House, siku moja baada ya Trump kumkosoa kwamba alishindwa kufikia makubaliano na Russia ambayo Trump anasema yangemaliza vita.

Makamu wa rais alisema atafanya juhudi kuhakikisha Ukraine inashinda vita ambavyo vimeingia mwaka wa tatu, na kupata amani.

Alimkosoa Trump, mpinzani wake wa chama cha Republican kwenye uchaguzi wa Novemba 5, bila kumtaja jina.

Trump baadaye alisema atakutana na Zelenskiy leo Ijumaa asubuhi katika jengo lake la New York, Trump Tower.

Trump na Zelenskiy walizungumza kwa simu mwezi Julai, lakini walikuwa hawajakutana ana kwa ana tangu Trump alipoondoka madarakani mwaka 2021.

“Mapendekezo hayo ni kama yale ya Rais wa Russia Vladimir Putin, acha tuwe wazi, sio mapendekezo kwa ajili ya amani. Bali, ni mapendekezo ya kujisalimisha, jambo ambalo ni hatari na lisilokubalika,” alisema.

Kabla ya ziara ya Zelesnkiy, utawala wa Marekani ulitangaza msaada mpya wa dola bilioni 8 kwa Ukraine.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii