RAIS William Ruto amekemea wakfu wa Ford Foundation akiihusisha na vurugu zilizoshuhudiwa nchini wakati wa maandamano yaliyopinga Mswada wa Fedha wa 2024 na jinsi utawala wa Kenya Kwanza unaendesha serikali.
“Mimi ninataka kuuliza watu wa Ford Foundation, wanatoa pesa kuchochea fujo ili wapate faida gani? Inaonekana hawana haja ya demokrasia kuwepo Kenya kwa sababu wanafadhili fujo. Tutawakashifu na kuwataka wawe wastaarabu ama waondoke,” alifoka Rais.
Ford Foundation ni shirika la hisani lenye lengo la kushughulikia masuala ya kijamii.
Lina makao yake makuu, jijini New York, Amerika.
Rais alizungumza haya Jumatatu, Julai 15, 2024 akiwa eneobunge la Kuresoi Kusini, Kaunti ya Nakuru alipozindua ujenzi wa soko la mazao mabichi ya Keringet.
“Vijana wetu hawana wakati wa shughuli zilizopitwa na wakati. Wale wanaowafadhili wasababishe machafuko wanafaa kujiaibikia,” alighadhabika Rais Ruto akihutubia umati.
Maandamano yaliyosukumwa na vijana wa kizazi cha Gen Z yalitikisa nchi Juni 25, 2024 na kuishia kusababisha maafa ya watu 42 huku waandamanaji wengine wakitekwa nyara.
Vijana hawa na Wakenya wengi walikuwa wanapinga sheria dhalimu ya ushuru huku wakishinikiza serikali iwajibike kwa kukithiri kwa ufisadi na utepetevu serikalini.
Juni 10, 2024 akiwa Kaunti ya Kajiado, Dkt Ruto alilaumu mashirika ya kigeni aliyodinda kuyataka akidai yalifadhili maandamano hayo.
“Na wale wanajaribu kufanya mambo kule ng’ambo sijui wapi kupangapanga (alilaumu mashirika ya kigeni kwa maandamano ya vurugu)…Ninataka kuwaambia Kenya ni nchi ya kidemokrasia,” alisema akiwaambia wakosoaji wake wasubiri uchaguzi mkuu wa 2027 wakabiliane naye.
Maandamano ya kupinga serikali yalimshurutisha Rais kuvunja baraza la mawaziri kisha kupisha kongamano la kitaifa kujenga upya serikali kuanzia Julai 15, 2024.
Kabla ya kuchukua hatua hii, Rais alisalimu amri ya matakwa ya wananchi na kudinda kutia saini Mswada wa Fedha 2024 kuwa sheria.