Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama amewaambia wanachama wenzake wa Democratic mjini Chicago kuwa kijiti kimekabidhiwa kwa Kamala Harris, na anatosha kuiongoza nchi hiyo.
Akihutubia wakati wa kumpigia debe Harris katika mkutano mkuu wa chama cha Democratic, Obama amesema Kamala ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Marekani, ndiye atawapigania Wamarekani. Obama amesema Harris yuko tayari kwa ajili ya kazi ya urais, na amekuwa akiyatumia maisha yake kuwapigania watu wasio na sauti. Aidha, Obama amewatolea wito Wamarekani kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi mwezi Novemba ili kumshinda Donald Trump.