Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza mlipuko wa ugonjwa wa mpox katika baadhi ya maeneo ya Afrika kuwa dharura ya kiafya ya umma.
Ugonjwa unaoambukiza sana – ambao zamani ulijulikana kama monkeypox – umeua takriban watu 450 wakati wa mlipuko wa awali huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Sasa umeenea katika maeneo ya Afrika ya kati na mashariki, na wanasayansi wana wasiwasi kuhusu jinsi aina mpya ya ugonjwa huo inavyoenea na kiwango chake cha juu cha vifo.
Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema uwezekano wa ugonjwa huo kuenea zaidi ndani ya Afrika na kwingineko “kunatia wasiwasi sana”.
“Kukabiliana na ugonjwa huu kwa namna iliyoratibiwa ni muhimu ili kusitisha janga hili na kuokoa maisha,” alisema.
Mpox huambukizwa kupitia mguso wa karibu, kama vile ngono, mguso wa ngozi hadi ngozi na kuzungumza au kupumua karibu na mtu mwingine.
Husababisha dalili kama za mafua, vidonda vya ngozi na inaweza kusababisha kifo, na kesi nne kati ya 100 husababisha kifo.
Kuna aina mbili kuu za mpox – Clade 1 na Clade 2.
Dharura ya awali ya afya ya umma, iliyotangazwa mwaka wa 2022, ilisababishwa na Clade 2 ambayo si kali. Hata hivyo, wakati huu ni Clade 1 mbaya zaidi – ambayo imeua hadi 10% ya wale wanaougua katika milipuko ya awali – idadi hii inaongezeka.
Tangu wakati huo, ugonjwa wa mpox umegunduliwa katika nchi nyingine za Afrika – ikiwa ni pamoja na Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kenya na Rwanda.