Iran imeukataa wito wa mataifa ya Magharibi wa kuacha vitisho vyake vya kulipiza kisasi dhidi ya Israel kwa mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa kundi la Hamas, Ismail Haniyeh.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kanaani, amesema Jumanne kuwa wito wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza hauna mantiki, wala mashiko ya kisiasa na unakinzana na kanuni za sheria za kimataifa.
Kwa mujibu wa Kanaani, wito wa mataifa hayo ambao haukulaani uhalifu wa kimataifa unaofanywa na Israel, unaitaka Iran isichukue hatua zozote za kuizuia Israel ambayo imekiuka uhuru wa mamlaka ya eneo lake.
Amesema Iran imedhamiria kuzuia mashambulizi ya Israel na kutoa wito kwa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza kupinga vita vya Gaza na Israel ambayo inachochea vita.
"Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutochukua hatua na uungaji mkono mkubwa wa kisiasa na kijeshi wa serikali za Magharibi kwa utawala wa Israel, ndiyo sababu kuu zinazoufanya mzozo wa Gaza kutanuka na kuwa wa kikanda," alisisitiza Kanaani.
Katika taarifa yake ya jana Jumatatu, Marekani na washirika wake wa Ulaya ziliitolea wito Iran na washirika wake kujizuia na mashambulizi dhidi ya Israel, na kuepusha kutanuka kwa mzozo.
Iran na washirika wake makundi ya Hamas na Hezbollah la Lebanon, wameishutumu Israel kwa kufanya mauaji ya Haniyeh. Hata hivyo, serikali ya Israel haijakiri kuhusika na mauaji hayo.
Wakati huo huo, wanajeshi wa Israel wamemuua kwa kumpiga risasi mwanaume wa Kipalestina wakati wa msako mkali wa kuvunja makaazi ya washukiwa wawili wa Kipalestina waliokuwa wamezuiliwa mapema Jumanne alfajiri katika Ukingo wa Magharibi, kwenye miji ya Ramallah na Al-Bireh.
Jeshi la Israel halikuweza kuthibitisha mara moja taarifa hizo zilizotolewa na maafisa wa wizara ya afya ya Palestina, pamoja na shirika la habari la Kipalestina la Wafa, ingawa imesema inazifuatilia kwa undani.