Wasiwasi inazidi kuongezeka kutokana na uwepo wa aina mpya ya maambukizo ya mpox, zamani yakifahamika kama monkeypox yaliogunduliwa nchini DR Congo na sasa katika mataifa jirani kuwa yanaweza kusambaa zaidi.
Maambukizo hayo mapya aina ya Clade Ib subclade ambayo yanaripotiwa nchini DRC tangu mwezi Septemba yametajwa kuwa hatari zaidi ikilinganishwa na ya awali ambapo yanasambazwa baina ya binadamu.
Jumapili ya wiki iliopita, shirika la afya duniani WHO lilitangaza kwamba linawazia kutangaza maambukizo ya Mpox kama janaga la kimataifa kama ilivyokuwa kwa mwaka wa 2022.
Aina hii ya Mpox kwa jina la Clade Ib imeripotiwa kusababisha kuchipuka kwa vidonda kwenye mwili wote kinyume na maambukizo ya awali ambapo ishara zilikuwa zikionekana kwenye kinye, uso na sehemu za siri za mgonjwa.
Kituo cha kudhibiti mgonjwa barani Afrika CDC, kimesajili visa 14,479 vinavyohusishwa na maambukizo hayo mapya pamoja na vifo 455 nchini DRC kufikia tarehe 3 ya mwezi Agosti.
Serikali ya DRC, mwezi uliopita ilithibitisha kuwepo kwa ongezeko la maambukizo ya Mpox.
Kwa mujibu wa mkuu wa shirika la MSF nchini DRC, Louis Albert Massing, maambukizo ya Mpox yalikuwa yametambuliwa katika kambi za wakimbizi karibu na Goma jijini Kivu Kaskazini.
Tayari Clade Ib imeripotiwa katika mataifa ya Uganda, Burundi, Rwanda kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO.
Mamlaka katika mataifa hayo ya Afrika Mashariki yamethibitisha uwepo wa maambukizo hayo, Burundi ikiwa imeripoti visa 127 bila ya kutaja aina ya Mpox.