Rais wa Bangladeshi Mohammed Shahabuddin amevunja bunge siku ya Jumanne, kulingana na msemaji wa rais, na kuwaridhisha wanafunzi waliomtimua Waziri Mkuu Sheikh Hasina. "Rais amelivunja Bunge," Shiplu Zaman amesema katika taarifa yake.
Uamuzi huo wa rais Mohammed Shahabuddin unafuatia maandamano ya ghasia katika siku za hivi karibuni, yaliyopelekea Waziri Mkuu Sheikh Hasina kukimbilia India.
Wanafunzi waliokuwa wakiandamana walitaka bunge livunjwe, kama vile chama kikuu cha upinzani, Bangladeshi Nationalist Party (BNP), ambacho kinataka uchaguzi ufanyike ndani ya miezi mitatu. Maandamano ya kupinga mfumo wa uajiri wa upendeleo katika utawala yamesababisha vifo vya watu 413 tangu mwanzoni mwa mwezi Julai kote nchini. Mkuu wa jeshi la Bangladesh, Jenerali Waker-Uz-Zaman, ambaye anatazamiwa kukutana na viongozi wa vuguvugu la wanafunzi siku ya Jumanne, alitangaza siku ya Jumatatu kuundwa kwa serikali ya mpito hivi karibuni.