Burkina Faso ilipitisha hati siku ya Jumamosi kuruhusu utawala wa kijeshi wa Kapteni Ibrahim Traoré, ambaye aliingia madarakani Septemba 2022 kupitia mapinduzi ya kijeshi, kusalia kwa miaka mitano zaidi kama mkuu wa nchi hii iliyoathiriwa na ghasia za wanajihadi.
"Muda wa mpito umewekwa kuwa miezi 60 kutoka Julai 2, 2024," amesema Kanali Moussa Diallo, mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mikutano.
Rais Traoré, ambaye hadhi yake inabadilika kutoka "rais wa mpito" hadi "rais wa Burina Faso", pia ataweza kujitokeza katika "chaguzi za urais, wabunge na manispaa ambazo zitafanyka" mwishoni mwa kipindi hiki, ameongeza kanali Diallo.
Mikutano hiyo ya kitaifa, iliyopangwa kumalizika siku ya Jumapili, ilileta pamoja wawakilishi wa mashirika ya kiraia, vikosi vya ulinzi na usalama na hata wabunge kutoka bunge la mpito siku ya Jumamosi. Vyama vingi vya kisiasa vilisusia hafla hiyo.
Katika mkataba mpya uliotiwa saini siku ya Jumamosi na Kapteni Traoré, "idadi" iliyotangazwa kwa vyama vya siasa kwa nafasi za ubunge katika bunge la mpito imeondolewa.
"Uzalendo" umewekwa kuwa kigezo cha kushiriki katika bunge hili au serikalini.
Burkina Faso, inayokumbwa na ghasia za mara kwa mara za wanajihadi ambazo zimesababisha vifo vya maelfu ya watu kwa takriban miaka kumi, ilikumbwa na mapinduzi mawili ya kijeshi mwaka 2022.
Mapinduzi ya kwanza, mnamo mwezi Januari, yalimweka Luteni-Kanali Paul Henri Sandaogo Damiba madarakani, kabla ya yeye mwenyewe kupinduliwa mnamo Septemba mwaka huo huo, na Kapteni Traoré.
Katika mchakato huo, katiba ilipitishwa wakati wa mikutano ya kwanza ya kitaifa, kumuweka rais, serikali, bunge la mpito la sheria (ALT) na kuweka kipindi cha mpito kwa miezi 21.
Kwa hivyo mpito huu ulipaswa kumalizika Julai 1, 2024, lakini mara kadhaa Kapteni Traoré alizungumzia ugumu wa kufanya uchaguzi kutokana na mazingira ya usalama nchini.