Raia wa Kenya aliyekuwa akiukwea Mlima Everest ameripotiwa kufariki wakati mwongozaji wake raia wa Nepali akiwa hajulikani alipo, akiwa mtu tatu kufariki kwenye mlima huo mrefu zaidi duniani msimu huu.
Joshua Cheruiyot Kirui, 40, na mwongozaji wake raia wa Nepali Nawang Sherpa, 44, walitoweka siku ya Jumatano asubuhi ambapo harakati za kuwatafuta zilianza rasimi kwenye mlima huo mwenye mita 8,849 sawa na futi 29,032.
Baada ya shughuli hiyo ya kuwatafuta, hatimaye mwili wa raia huo wa Kenya umepatikana kwenye eneo hilo wakati mongozaji wake akiwa hajulikani aliko kwa mujibu wa taarifa kutoka mamlaka ya utali katika eneo hilo.
Zoezi ya kumtafuta mkwea milima mwengine raia wa Uingereza mwenye umri miaka 40 pamoja na muongozaji wao mwenye umri wa miaka 21, raia wa Nepal limekuwa likiendelea tangu siku ya Jumanne walipotoweka baada ya barafu kuporomoka wakati wakiuukwea mlima Everest.
Jumatatu ya wiki hii, mkwea mlima mwengine raia wa Romania aliripotiwa kufariki katika hema lake wakati akitarajiwa kuupanda mlima wa Lhotse ambao unapatikana kwenye njia sawa ya kuelekea kwenye mlima Everest, mlima wa nne kwenye urefu zaidi duniani.
Mapema mwezi huu, wapanda milima wawili kutoka Mongolia walitoweka baada ya kufika kilele cha Everest kabla ya kupatikana wakiwa wamefariki.
Mwaka jana, zaidi ya watu 600 walifanikiwa kufika kwenye kilele cha mlima Everest, vifo 18 vikiripotiwa.