Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak anafanya ziara Marekani kuanzia leo yenye lengo la kuimarisha mshikamano baina ya madola hayo mawili washirika hususani kwenye masuala ya uchumi na teknolojia mamboleo.
Sunak ambaye aliwasili mjini Washington usiku wa kuamkia leo amepangiwa kukutana na rais Joe Biden kesho Alhamisi kwa mazungumzo yatakayogusia pamoja na mambo mengine mshikamano wa Uingereza na Marekani wa kuisadiai Ukraine katika vita vinavyoendelea.
Waziri Mkuu Sunak amesema analenga pia kuimarisha mahusiano ya Uingereza na Marekani kwenye nyanja za uchumi kama ilivyo kwenye eneo la ulinzi na usalama.
Ajenda nyingine muhimu itakuwa ni njia za kudhibiti matumizi ya teknolojia ya akili bandia baada ya wataalamu kadhaa wa sekta hiyo kutoa hadhari kwamba inaweza kuleta kitisho kwa ustawi wa binadamu ndani ya miaka michache inayokuja.