Jeshi la Uganda laghadhabishwa na vikwazo vya Marekani dhidi ya mkuu wake wa ujasusi

Jeshi la Uganda limelalamikia vikwazo vya kifedha vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Meja Jenerali Abel Kandiho, mkuu wa ujasusi wa kijeshi wa nchi hiyo.

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda lilisema katika taarifa yake Jumanne kwamba vikwazo hivyo viliwekwa bila kufuata utaratibu na kwa kupuuza kabisa kanuni ya kusikilizwa kwa haki.

Ilisema imesikitishwa kwamba hatua kama hiyo imechukuliwa na nchi ambayo Uganda inaiona kuwa rafiki na mshirika mkubwa.

Katika kuweka vikwazo hivyo, Hazina ya Marekani ilisema kuwa Bw Kandiho na maafisa wengine wa kijasusi wa kijeshi walikamata, kuwaweka kizuizini na kuwanyanyasa kimwili watu "kutokana na utaifa wao, mitazamo ya kisiasa, au ukosoaji wa serikali ya Uganda".

Ilisema kwamba waliokamatwa "walipigwa na kufanyiwa vitendo vingine vya kutisha... ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia na kupigwa na umeme, mara nyingi kusababisha majeraha makubwa ya muda mrefu na hata kifo".

Vikwazo hivyo vimekuja baada ya ripoti kuwa programu za ujasusi zilizotengenezwa na kampuni ya mtandao ya Israel ya NSO Group, zilitumika kudukua simu za wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani nchini Uganda.

Mwezi Aprili, Marekani iliweka marufuku ya usafiri dhidi ya maafisa wa Uganda ikisema walihusika na ukiukaji wa haki za binadamu unaohusishwa na uchaguzi mkuu wa Januari.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii