Tanzania yafunga kambi ya wakimbizi wa Burundi.

Kambi ya Mtendeli, moja ya kambi tatu za Tanzania zinazohifadhi wakimbizi wa Burundi imefungwa kabisa, baada ya zaidi  ya wakimbizi elfu 19 wa mwisho waliokuwa  katika  kambi hiyo kuhamishiwa kwenye kambi ya Nduta Jumatatu.

Maafisa wanaohusika na idara ya wakimbizi nchini Tanzania wanasema hatua ya kufunga kambi hiyo imechukuliwa ili kushughulikia ipasavyo suala la usalama ambao ulikuwa ukivurugika mara kwa mara ndani ya kambi.

Maafisa hao wanasema usalama utaimarishwa ikiwa zitabaki kambi mbili pekee, ile ya Nyarugusu na hiyo ya Nduta ambayo ndiyo kambi inayohifadhi idadi kubwa ya wakimbizi wa Burundi.

Taarifa zinaendelea kusema kwamba viongozi wanapanga pia kuwahamisha wakimbizi wote wa Burundi wanaopatikana katika kambi ya Nyarugusu na kuwapeleka kwenye kambi ya Nduta. Wakimbizi kutoka Congo ndio watabaki katika kambi ya Nyarugusu, taarifa zimeendelea kusema.

Wakimbizi elfu 3 waliokuwa Mtendeli walirejea nyumbani kwa hiara hiyo tangu mwezi Julai mwaka huu.

Kufikia tarehe 31 Oktoba mwaka huu, zaidi ya wakimbizi wa Burundi laki 2 na elfu 60 ndio walikuwa wanapiga kambi katika nchi nne ambazo ni Tanzania, Rwanda, Uganda na DRC, Tanzania pekee ikiwa inahifadhi zaidi ya wakimbizi laki 1 na elfu 20, kulingana na takwim za shirika la Umoja wa mataifa linalohudumia wakimbizi (UNHCR)


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii