Mshukiwa wa mauaji ya mwandishi wa habari akamatwa

Mwanaume mmoja raia wa Saudi Arabia anayeshukiwa kuhusika na mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi amekamatwa nchini Ufaransa, ripoti zinasema. 

Khaled Aedh Al-Otaibi alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Charles-de-Gaulle siku ya Jumanne, vyombo vya habari vya Ufaransa vinaripoti. 

Yeye ni mmoja wa Wasaudia 26 wanaotafutwa na Uturuki kutokana na mauaji ya mwanahabari huyo. 

Mlinzi huyo wa zamani wa kifalme wa Saudi mwenye umri wa miaka 33 alikuwa akisafiri kwa jina lake mwenyewe na kuwekwa katika kizuizi cha mahakama, redio ya RTL ilisema. 

Khashoggi, mkosoaji mashuhuri wa serikali ya Riyadh, aliuawa katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul Oktoba 2018. 

Saudi Arabia ilisema mwandishi huyo wa zamani wa gazeti la Washington Post aliuawa katika "operesheni mbaya" na timu ya maajenti waliotumwa kumshawishi arejee katika ufalme huo. 

Lakini maafisa wa Uturuki walisema maajenti hao walifanya kazi kwa amri kutoka ngazi za juu za serikali ya Saudia.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii