Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis leo amekitembelea kwa mara nyingine kisiwa cha Lesbos nchini Ugiriki eneo ambalo lilikuwa kitovu cha wimbi la wahamiaji miaka 6 iliyopita na kuitaja tabia ya kuwapuuza wahamiaji kuwa ni "kwenda mrama kwa ustaarabu" duniani. Papa Francis ambaye alitumia muda wa saa mbili kukizuru kisiwa hicho chenye kiasi waomba hifadhi 2,200 ameonya kuwa bahari ya Mediterrania inageuka kuwa eneo la makaburi lisilo na mawe na ulimwengu haujabadilika vya kutosha linapokuja suala la uhamiaji. Alipokitembelea kisiwa cha Lesbos mwaka 2016, Papa Francis aliwachukua wahamiaji 12 kutoka Syria na kuondoka nao kwa kutumia ndege rasmi inayomsafirisha. Ziara yake kwenye kisiwa hicho ni sehemu ya ziara yake ya siku tano nchini Cyprus na Ugiriki na imefanyika siku moja tangu alipotoa mataashi makali ya kukemea siasa za kizalendo alizosema zinatishia ustawi na demokrasia barani Ulaya