Rais mteule Faye awaalika wawekezaji wa kigeni

Senegal itafanya ukaguzi wa sekta za mafuta, gesi na madini, rais mteule wa Senegal Bassirou Diomaye Faye alisema Jumatano katika hotuba kwa taifa kwa njia ya televisheni, huku akiwahakikishia wawekezaji kwamba wamekaribishwa nchini. 

Faye alimshinda kwa kishindo mgombea wa muungano wa vyama tawala kwenye uchaguzi wa mwezi Machi, ikiashiria matumaini makubwa ya mabadiliko katika nchi hiyo yenye watu milioni 18.

Ukaguzi huo ni moja ya hatua za kwanza za sera kutangazwa tangu kuapishwa kwa mkaguzi huyo wa zamani wa kodi mwenye umri wa miaka 44 siku ya Jumanne.

“Uporaji wa maliasili zetu ambazo kwa mujibu wa katiba ni mali ya wananchi, utapewa kipaumbele maalum na serikali yangu,” alisema.

“Nitatangaza umiliki bora wa kampuni za uchimbaji na ukaguzi wa sekta ya madini, mafuta na gesi,” aliongeza.

Hakutoa maelezo zaidi, lakini alitaka kuwahakikishia wawezekazaji, ambao alisema “wanakaribishwa nchini Senegal.”

“Haki za wawekezaji zitalindwa kila siku, vile vile maslahi ya serikali na wanainchi,” alisema.

Uzalishaji wa kwanza wa mafuta ghafi nchini Senegal unatarajiwa kuanza katikati ya mwaka huu wa 2024. Mradi wa mafuta na gesi wa Sangomar unaosimamiwa na Woodside Energey WDS.AX unatarajiwa kuzalisha takriban mapipa 100,000 kwa siku.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii