Shambulio la ndege isiyokuwa na rubani laua watu 12 kaskazini mashariki mwa Sudan

Shambulio la ndege isiyokuwa na rubani liliua watu 12 na kujeruhi wengine 30 Jumanne katika mji wa kaskazini mashariki mwa Sudan wa Atbara, ambao kufikia sasa, ulikuwa umeepuka vita vya kikatili, madaktari na mashahidi wamesema.

Sehemu kubwa ya Sudan imekumbwa na vita vibaya vya karibu mwaka mmoja kati ya jeshi la serikali na wanamgambo wa kikosi cha Rapid Support Forces (RSF).

“Moto ulizuka baada ya shambulio la ndege isiyokuwa na rubani wakati wa Iftar,” shahidi mmoja alisema kwa njia ya simu, akimanisha chakula cha jioni wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Chakula hicho ambacho kilikuwa kimeandaliwa kwenye kambi ya kundi la wanamgambo la Baraa, ambalo linapigana upande wa jeshi la Sudan, kiliwaleta pamoja raia na wapiganaji, mkazi mwingine ameiambia AFP.

Wakazi walipatwa na wasiwasi kutokana na mlipuko mkubwa huko Atbara, mji unaopatikana umbali wa kilomita 300 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Khartoum, chanzo hicho kilisema.

Miili ya watu 12 waliouawa, na wengine 30 waliojeruhiwa walifikishwa kwenye hospitali ya Atbara, chanzo cha madaktari kilisema, na kusahihisha idadi ya awali ya vifo bila pamoja na hivyo kufafanua ikiwa walikuwa wapiganaji au raia.

Vita hivyo ambavyo vilizuka tarehe 15 Aprili mwaka jana, vimeua maelfu ya watu na kuhamisha kwenye makazi yao zaidi ya watu milioni 8.5 ndani ya nchi na nje ya mipaka, kulingana na Umoja wa mataifa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii