Ujasiri wa maisha, mama lishe hadi dereva

“Nilizoea kuwa mkarimu kwa wateja wakati nafanya biashara ya mama ntilie kwakuwa lazima uwe mchangamfu ili uwavute wateja, lakini moyo wangu umebadilika baada ya kuanza kazi ya udereva wa maroli masafa marefu.

“Kwenye nchi za wenzetu ukarimu si jambo linalozingatiwa na watu kama ilivyo kwetu, mara nyingi tunakutana na watu wenye ukatili, yaani mtu yuko tayari kufanya chochote ili apate pesa hivyo kuua si kitu cha ajabu kukabiliana nao ni lazima na wewe uwe na roho ngumu,”.

Hivyo ndivyo anavyoanza kuelezea Miriam Fabian (32) dereva wa malori ya mizigo yanayofanya safari za Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

DRC, akiwa amefanya kazi hiyo kwa miaka sita baada ya kuachana na biashara ya mama ntilie.

Katika mahojiano aliyofanya na gazeti hili Miriam anaeleza kuwa hali ya kukosekana amani na utulivu nchini DRC kunawafanya hata wageni wanaoingia katika nchi hiyo kuwa hatarini.

Kama ilivyo kwa wageni wengi, akiwa njiani ndani ya nchi hiyo huwa anakumbana na vikwazo kadha wa kadha ambavyo wakati mwingine vinamlazimu kupambana na waharifu wanaojaribu kuteka magari ili wajipatie fedha kutoka kwa madereva.

“Ukiangalia kwenye gari yangu pale mbele nimeficha mapanga, kuna muda unalazimika kuuvua ubinadamu ili uweze kujilinda maana kinyume na hapo wewe ndiye unaweza kupoteza maisha.

Mara nyingi nimekutana na matukio ya kupambana njiani, kule kuna vijana wenye fujo wanaweza kuzuia gari wakataka uwape fedha sasa hapo itategemea na namna atakavyokuja, akija kwa utulivu utazungumza naye na kumpatia kama unazo ila akija kishari ndio unalazimika kujihami kwa silaha,”

Akisimulia kisa kimoja alichowahi kukutana nacho, “Nakumbuka ilikuwa, safari yangu ya pili Congo, gari yangu iliharibika hivyo nikakaa pale kwa muda mrefu sasa siku hiyo akaja kijana anataka nimpe hela alikuja kwa shari nikatoa panga nikapamba naye.

“Baada ya kumshambulia yule wakaja wengine tukabishana hivyo hivyo nikawapa pesa lakini pia hawakuridhika, mmoja wao akang’ang’ania kwenye kioo basi niliendesha gari akadondoka nacho,”.

Pamoja na changamoto hizo Miriam husafiri peke yake kwenye gari na hana tatizo na hilo kwa kuwa anaamini kazi aliomba mwenyewe hivyo anatakiwa kuitumikia kama alivyoiomba.

Kabla ya udereva, mwaka 2014 Miriam ambaye ni mama wa watoto watano alikuwa akifanya biashara ya kupika na kuuza chakula katika mgahawa uliokuwa mjini Igunga pembezoni mwa barabara ya Tabora Singida.

Eneo aliloweka mgahawa huo ilikuwa jirani na yanapoegeshwa malori hivyo wateja wake wakubwa walikuwa madereva wa magari hayo.

Kutokana na umahiri wake kwenye upishi alijikuta akiwavuta madereva wengi kula chakula kwenye mgahawa wake na ndipo alipopata nafasi ya kuzungumza nao kwa kina kuhusu kazi hiyo aliyokuwa anaitamani.

“Wakati wa utoto wangu nyumbani kwetu kulikuwa na trekta basi nikiwa darasa la nne nilijifunza kuliendesha hadi nikawa fundi kabisa, sasa nilivyokuwa pale mgahawani, ukaribu na madereva ukanifanya nitamani kuendesha magari.

“Niliwaeleza kiu yangu walinitia moyo na kunihamasisha kujifunza kuendesha gari, kaka yangu ndiye aliyenipa msukumo zaidi wa kujifunza baada ya kuniambia kuwa siku hizi hakuna kazi ya mwanamke wala mwanaume, ushauri huo uliniingia kichwani nikaanza kujifundisha,”

Kutokana na uzoefu wake katika kuendesha trekta haikumchukua muda mrefu kumudu kuendesha lori na hatimaye akawa dereva.

Mei 2016 alijiunga na Chuo cha Veta Kihonda mkoani Morogoro kusoma kozi maalumu ya udereva wa malori na hatimaye akapata cheti na leseni.

Heka heka za kutafuta ajira zikaanza ndipo alipokuja jijini Dar es Salaam kujaribu bahati yake kwenye kampuni mbalimbali na alifanikiwa kuanza kwa kupata nafasi ya kujifunza kwa vitendo kabla ya kuajiriwa rasmi.

Safari yake ya kwanza baada ya kuajiriwa ilikuwa mwaka 2018 alipopangiwa kwenda Burundi ambapo hofu na furaha vilitawala kichwani mwake akifurahia kuajiriwa huku akihofia kama ataweza kumudu jukumu hilo.

“Wakati nikiwa najifunza kwa vitendo nilikuwa napata safari kadhaa za kwenda Burundi hivyo njia nilikuwa naifahamu vyema lakini bado nilikuwa na hofu kweli nitaweza yaani mimi ndio nimekabidhiwa gari kama dereva kwa kweli ilinichukua muda kuamini.

“Furaha niliyokuwa nayo siku ile ilibidi nimshukuru Mungu kwa kujifanyia sherehe ndogo bila kumhusisha mtu, nilichinja kuku nikapika pilau sikumwambia yeyote kuwa nafanya hivyo kujipongeza ilikuwa siri ya moyo wangu,” anasema.

Huo ndio ukawa mwanzo wa maisha ya barabarani kwa Miriam ambayo hadi sasa amefanya kwenye kampuni mbili na amekuwa dereva wa kutegemewa na kuaminika kwenye kampuni anayoifanyia.

Tofauti na ilivyo wanawake wengi wanaofanya shughuli za aina hiyo kulazimika kuvaa mavazi ya kiume ili wawe huru, Miriam anajulikana zaidi kama dada wa magauni.

Mama huyu huendesha gari akiwa amevalia gauni kwa kile anachodai kuwa humfanya kuwa huru zaidi na kufuata misingi ya malezi aliyolelewa.

“Mimi mama wa kinyamwezi na suruali wapi na wapi yani hata nikivaa, itakuwa ndani ya gauni, kwetu nimelelewa mwanamke anatakiwa kujisitiri hivyo lazima nivae nguo pana kama gauni au dela.

Nguo za aina hiyo hazijawahi kunisumbua na siku zote naendesha hivyo ndiyo maana hata wenzangu wengine wananiita dada wa magauni, bado nina yale mawazo ya mwanamke anayejiheshimu anatakiwa kuheshimu mwili wake,”.

Anasema kama ilivyo kazi nyingine udereva nao una changamoto zake hivyo ni muhimu kwa mwanamke anayetaka kufanya kazi hiyo kujiandaa kwa kuwa dereva aliyekamilika.

“Ukiwa dereva na umeaminiwa umekabidhiwa gari lazima uweke uanamke wako pembeni, vaa ujasiri ufanye kazi yako kwa ufanisi na umakini mkubwa.Inaweza kutokea uko porini tairi likapata pancha, hivyo lazima ujue kubadilisha, ukisema uchanganyikiwe kazi yako inaweza kuwa ngumu.

“Hii kazi haiitaji huruma wala haitakiwa kuweka hisia mbele hutakiwi kuogopa lazima ukabiliane na kinachokuja mbele yako, sisi tunaofanya safari za Congo tunasafiri katika mazingira hatarishi mno ndiyo maana sio ajabu mimi kushika panga kumkata nalo anayejaribu kutaka kunidhuru,” Anaongeza, “Huku sheria huwa ni moja ukijifanya laini laini wewe ndiye utakayeshambuliwa sasa yale mambo ya umama huwa tunayaweka kando kidogo tukiwa barabarani, nikirudi nyumbani nakuwa mama na mwanamke kwa mwanaume wangu,”.

Kati ya madereva 11 wa masafa wa kampuni ya YAATE Investment, Miriam ni mwanamke pekee aliyeaminiwa kupewa jukumu hilo akizungukwa na wanaume 10.

Ramadhan Mbughi ambaye ni fundi mkuu wa kampuni hiyo anamtaja Miriam kama dereva tegemezi na anayeaminiwa kutokana na umakini wake awapo barabarani.

“Huyu anatupa funzo kubwa kwanza mwanamke peke yake halafu anafanya kazi nzuri kuliko hata hawa vijana wa kiume, anaendesha gari vizuri hatujawahi kupata kesi wala harasa yoyote kubwa.

“Tumejifunza kwamba siku hizi wanawake wanaweza na kama inavyosema kwamba hawa mama zetu ni waaminifu, huyu analidhihirisha hilo hana tamaa, hana kesi za mafuta kwa kifupi anafanya tufikirie kuwa na wanawake wengi zaidi madereva kwenye kampuni kuliko wanaume,” anasema Mbughi.

Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa) Elias Lukumay alisema licha kwamba wanawake sio wengi kwenye kazi hiyo, lakini wameonekana kuwa na mafanikio makubwa.

“Japo sio kampuni zote zilizowaajiri wanawake lakini tunapendelea kuwaajiri kwa sababu wameonekana kuwa na umakini mkubwa na ni waaminifu, kwa hiyo tunapunguza ajali. Unajua wanawake wana asili ya kutunza vitu.

Pia wanawake wanajali familia, kwa hiyo ukimtunza mwanamke umeitunza familia,” alisema Lukumay.



Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii